Mkutano wa dharura wa kilele wa Nchi za Kiarabu waanza nchini Misri kujadili ujenzi upya wa Gaza bila watu kuhamishwa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 05, 2025

Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuhudhuria Mkutano Maalum wa Kilele wa Nchi za Kiarabu kwa ajili ya Palestina katika Mji Mkuu Mpya wa Utawala, Misri, Machi 4, 2025. (Ikulu ya Misri/ kupitia Xinhua)

Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuhudhuria Mkutano Maalum wa Kilele wa Nchi za Kiarabu kwa ajili ya Palestina katika Mji Mkuu Mpya wa Utawala, Misri, Machi 4, 2025. (Ikulu ya Misri/ kupitia Xinhua)

CAIRO - Mkutano wa dharura wa Kilele wa Nchi za Kiarabu umeanza katika Mji Mkuu Mpya wa Utawala wa Misri jana Jumanne, ukikusanya viongozi na wajumbe wa Nchi za Kiarabu vilevile wawakilishi kutoka mashirika ya kimataifa ili kujadili maendeleo ya hivi karibuni katika Palestina na ujenzi upya wa Gaza.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo, Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi amesema Misri imefanya kazi, kwa ushirikiano na Palestina na taasisi za kimataifa, kuandaa mpango kamili wa kuijenga upya Gaza bila ya kuhamisha wakaazi wake.

Mpango huo utaanzia awamu ya mapema ya uimarishaji wa hali ili kushughulikia mahitaji ya dharura ya kibinadamu mjini Gaza na kuendelea na awamu ya ujenzi upya, amesema, akitoa wito wa kupitisha na kuunga mkono mpango huo.

“Mpango huo lazima uende sambamba na njia dhahiri ya kuelekea amani inyozingatia mambo ya kisiasa na usalama, ambapo nchi za kikanda zinashiriki kwa kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa ili kufikia suluhu ya haki na kamili ya suala hilo la Palestina,” amesema.

Sisi amesema Misri itaandaa mkutano wa ujenzi upya wa Gaza mwezi Aprili.

Amesema Misri, kwa ushirikiano na Palestina, imeunda kamati ya utawala ya wataalamu na wajuzi wa kujitegemea wa Palestina ili kusimamia operesheni ya misaada mjini Gaza na kusimamia kwa muda eneo hilo kwa maandalizi ya kurejeshwa kwa Mamlaka ya Palestina mjini Gaza.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Ahmed Aboul-Gheit amesisitiza kuwa ghasia hazitakoma kama uvamizi wa Israel hautakoma, na mtazamo wowote haramu wa eneo hilo hautakubaliwa.

“Ghasia hazitakomeshwa kwa kufukuza Wapalestina, na ujenzi upya wa Gaza unawezekana kwa wakati huohuo kubakisha wakazi wake kwenye ardhi yao,” amesema.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesisitiza Umoja wa Mataifa upo tayari kuunga mkono mpango huo ulioandaliwa na Misri, akisisitiza kwamba Gaza inapaswa kubaki kama sehemu ya Palestina.

Akiielezea hali ya Gaza kuwa "ya kutisha," Guterres ametoa wito wa kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia katika eneo hilo.

Siku ya Jumapili, Israel iliamua "kuzuia uingiaji wowote wa bidhaa na misaada ndani ya Gaza" ili kuishinikiza Hamas kukubali pendekezo jipya la kuongeza muda wa awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusimamisha mapigano yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili mwezi Januari.

Mkutano huo wa dharura baadaye utajadili mpango huo ulioandaliwa na Misri.

Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi (wa kwanza kulia) akihutubia katika Mkutano Maalum wa Kilele wa Nchi za Kiarabu kwa ajili ya Palestina katika Mji Mkuu Mpya wa Utawala, Misri, Machi 4, 2025. (Ikulu ya Misri/ kupitia Xinhua)

Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi (wa kwanza kulia) akihutubia katika Mkutano Maalum wa Kilele wa Nchi za Kiarabu kwa ajili ya Palestina katika Mji Mkuu Mpya wa Utawala, Misri, Machi 4, 2025. (Ikulu ya Misri/ kupitia Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha