

Lugha Nyingine
China yaonya kwamba pendekezo la Marekani kutoza ada za bandari kwa meli za China linaweza kwenda kinyume cha matarajio yake
BEIJING - Wizara ya Biashara ya China imesema kuwa kutoza ada kwa meli za China zinazoingia kwenye bandari za Marekani kutavuruga minyororo ya usambazaji bidhaa duniani na kwenda kinyume cha matarajio yake ya uchumi na nafasi za ajira za Marekani.
He Yadong, msemaji wa wizara hiyo amesema hayo jana Alhamisi kwenye mkutano na waandishi wa habari alipokuwa akitoa maoni yake kuhusu pendekezo la Ofisi ya Mwakilishi wa Biashara wa Marekani (USTR) la kutoza ada hizo.
Msemaji huyo amesema, kama Marekani itasisitiza kuweka ada hizo za bandari, itaongeza gharama za usafiri duniani na kuvuruga utulivu wa minyororo ya usambazaji bidhaa duniani.
"Hatua kama hizo pia zinaweza kuongeza shinikizo la ndani la mfumuko wa bei nchini Marekani, kudhoofisha nguvu ya ushindani duniani ya bidhaa za Marekani, na kudhuru watumizi wake na biashara za Marekani,” msemaji huyo ameonya.
Ofisi hiyo ya USTR Februari 21 ilitangaza kwamba iko katika kukusanya maoni ya umma kuhusu hatua hizo pendekezwa katika uchunguzi wa Kifungu cha 301 kuhusu sekta ya bahari, uchukuzi na ujenzi wa meli ya China, ikiwemo kutoza ada hizo za bandari.
“Uchunguzi wa Kifungu cha 301 wa Marekani ni kitendo halisi cha maamuzi ya upande mmoja na kujilinda ambacho kinakiuka sana sheria za Shirika la Biashara Duniani,” amebainisha.
Msemaji huyo amesema, China inaitaka Marekani kuheshimu ukweli wa mambo na sheria za pande nyingi, na kujiepusha kwenda mbali zaidi katika njia potofu, na China itafuatilia kwa umakini zaidi hatua hizo za Marekani, na itachukua hatua za lazima ili kulinda haki na maslahi yake halali.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma