Mkutano wa Macron na Trump waonesha mgawanyiko juu ya Ukraine kati ya Ulaya na Marekani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 26, 2025

Rais Donald Trump wa Marekani (kulia) akipeana mkono na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House mjini Washington, D.C., Marekani, Februari 24, 2025. (Xinhua/Hu Yousong)

Rais Donald Trump wa Marekani (kulia) akipeana mkono na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House mjini Washington, D.C., Marekani, Februari 24, 2025. (Xinhua/Hu Yousong)

PARIS/WASHINGTON - Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, baada ya mazungumzo ya kina na viongozi wa Ulaya katika siku chache zilizopita, amekutana na mwenzake wa Marekani Donald Trump katika Ikulu ya White House siku ya Jumatatu katika jitihada ya kuifanya sauti ya pamoja ya Ulaya kuhusu mgogoro wa Ukraine kusikika.

Licha ya hali tulivu ya nje, mkutano huo umethibitisha mgawanyiko dhahiri kati ya Ulaya na Marekani juu ya namna ya kufikia suluhu jumuishi kuhusu mgogoro huo.

Mgawanyiko dhahiri

Trump na Macron Jumatatu wamekubaliana juu ya kufikia amani ya kudumu kati ya Ukraine na Russia, lakini Macron amekanusha hadharani madai ya Trump kwamba "hali haikuwa ya haki" kwa Marekani kuhusu namna nchi hiyo na washirika wake wa Ulaya walivyotoa msaada kwa Ukraine.

"Ili tu muelewe, Ulaya inaikopesha Ukraine pesa hizo. Wanarejeshewa pesa zao," Trump akirejelea hoja ya juhudi zinazoendelea za Marekani kuishinikiza Ukraine kutia saini makubaliano ambayo yataipa Marekani haki ya kuchimba madini adimu ya Ukraine kama njia ya kurejesha fedha za msaada zilizotolewa na Marekani kwenye mgogoro huo.

Huku akimshika mkono Trump ili kuingilia kati, Macron amesema, "Hapana, kiukweli, kuwa wazi kabisa, tulilipa. Tulilipa asilimia 60 ya juhudi zote." Ameendelea kufafanua kwamba misaada ya Ulaya kwa Ukraine ilipangiliwa sawa na misaada ya Marekani. "Ilikuwa kama Marekani: mikopo, dhamana, misaada."

Akipuuza uingiliaji kati huo wa Macron, Trump amesema, "Kama mnaamini hivyo, ni sawa kwangu. Wanarudishiwa pesa zao, na sisi haturudishiwi. Lakini sasa tunarudishiwa."

Kutamani utajiri wa madini wa Ukraine

Siku ya Jumatatu, Trump alisema kwamba atakutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky "wiki hii au ijayo" katika Ikulu ya White House, na kwamba makubaliano ya mwisho kuhusu "madini adimu na mambo mengine" yalikuwa karibu sana.

Kwa upande mwingine, Kamishna wa Ulaya wa Mikakati ya Kiviwanda Stephane Sejourne alisema Jumatatu kwamba katika ziara yake mjini Kiev, pamoja na Rais wa Kamisheni ya Ulaya Ursula von der Leyen, amewapa ofa maafisa wa Ukraine ya makubaliano ya kunufaishana juu ya madini muhimu.

"Nyenzo 21 kati ya 30 muhimu ambazo Ulaya inahitaji zinaweza kutolewa kutoka Ukraine kama sehemu ya ushirikiano wa kunufaishana," Sejourne amesema baada ya mkutano na maafisa wa Ukraine, Shirika la Habari la AFP limeripoti.

Bendera za Umoja wa Ulaya (EU) na Ukraine zikipepea katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji, Februari 24, 2025. (Xinhua/Zhao Dingzhe)

Bendera za Umoja wa Ulaya (EU) na Ukraine zikipepea katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji, Februari 24, 2025. (Xinhua/Zhao Dingzhe)

Mshirika imara zaidi

Kwenye mazungumzo yake hayo na Trump mjini Washington, Macron alisema kuwa Ulaya iko tayari kuwa mshirika imara zaidi na kutoa mchango mkubwa zaidi katika masuala ya ulinzi.

"Kama Watu wa Ulaya, tunayo dhamira ya kuwa washikadau katika dhamana hizi za usalama," Macron amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha