Uholanzi kurudisha sanamu na vyombo vya shaba vya Benin vilivyoibwa kutoka Nigeria

(CRI Online) Februari 24, 2025

Uholanzi imesema itarudisha sanamu na vyombo 100 vya shaba vya Benin vilivyoporwa na wanajeshi wa Uingereza kutoka Nigeria mwishoni mwa Karne ya 19, ambavyo hatimaye viliishia kwenye jumba la makumbusho la Uholanzi.

Maelfu ya sanamu na nakshi za kitamaduni ziliporwa wakati wa uharibifu mkali wa mji wa Benin, katika jimbo la sasa la Edo nchini Nigeria, mwaka 1897.

Sanamu hizo ziliuzwa, baadhi kwa wakusanyaji binafsi na nyingine kwa makumbusho kama vile Jumba la Makumbusho la Wereld nchini Uholanzi, ambalo limekuwa likionyesha kazi hizo za sanaa kwa miongo kadhaa sasa.

Kurejeshwa kwa kazi hizo 119 za sanaa, kumeelezwa na mkurugenzi mkuu wa Kamisheni ya Taifa ya Makumbusho na Miundombinu ya Kale ya Nigeria (NCMM) Bw. Olugbile Holloway, kuwa ni urejeshwaji wa idadi kubwa zaidi wa vitu vya kale vya Benin.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha