

Lugha Nyingine
China yatoa wito wa usimamizi wa dunia wenye haki, ushirikiano imara zaidi wa pande nyingi
JOHANNESBURG - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema China inatoa wito wa kujenga mfumo wa usimamizi wa dunia wenye haki na usawa na kuhimiza ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja.
Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), ametoa kauli hiyo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari vya China kuhusu ziara yake nchini Uingereza na Ireland, kuhudhuria Mkutano wa 61 wa Usalama wa Munich (MSC) nchini Ujerumani, kuongoza mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, na kuhudhuria Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Kundi la nchi 20 (G20) nchini Afrika Kusini.
"China itachukua maadhimisho ya miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa kama fursa ya kushirikiana na pande mbalimbali ili kupata hekima kutoka kwenye historia, kuingia katika zama mpya ya ushirikiano wa pande nyingi, kujenga mfumo wa usimamizi wa dunia wenye haki na usawa, na kuhimiza ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja," Wang amesema.
Wakati mazingira ya sasa ya kimataifa yakipitia mageuzi na misukosuko, huku kukiwa na kuongezeka kwa nakisi za amani, maendeleo na utawala, usimamizi wa dunia umefikia njia panda ya kihistoria, amesema, akiongeza kuwa jumuiya ya kimataifa ina matarajio makubwa juu ya jinsi inavyoimarisha jukumu la Umoja wa Mataifa na kwa pamoja kushughulikia changamoto za kimataifa na maeneo ya kikanda yenye migogoro.
Amesema, ikiwa nchi mwenyekiti wa zamu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi wa Februari, China iliongoza mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu "Kutekeleza Ushirikiano wa Pande Nyingi, Kuufanyia Mageuzi na Kuuboresha Usimamizi wa Dunia" ili kusisitiza matarajio ya awali ya Umoja wa Mataifa, kujenga maelewano juu ya ushirikiano wa pande nyingi na kuongeza kasi mpya katika kuimarisha usimamizi wa dunia.
Kuhusiana na mkutano wa mwaka huu wa MSC ulioangazia dunia yenye ncha nyingi, Wang amesema licha ya changamoto ngumu zinazoikabili dunia, amani, maendeleo na ushirikiano wa kunufaishana vinaendelea kuwa mwelekeo usio na mbadala wa nyakati hizi, akiongeza kuwa mabadiliko ya kihistoria kuelekea dunia yenye ncha nyingi na utandawazi wa kiuchumi hayawezi kurudishwa nyuma.
Akibainisha kuwa Mkutano wa Kilele wa Viongozi Wakuu wa G20 utafanyika katika Bara la Afrika kwa mara ya kwanza mwezi Novemba mwaka huu, Wang amesema ni "wakati wa Afrika" kwa vyote G20 na usimamizi wa dunia, ikionyesha mabadiliko ya kihistoria katika nyanja ya kimataifa kisiasa na kiuchumi na kubeba umuhimu mkubwa.
"China itatoa mchango mkubwa na wa kiujenzi katika ushirikiano wa G20, kuunga mkono bila kuyumba urais wa Afrika Kusini, na kuhimiza pande zote kujikita katika kaulimbiu ya 'Umoja, Usawa na Uendelevu' ili kukidhi matarajio ya pamoja ya Nchi za Kusini” Wang amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma