Macron kufanya ziara nchini Marekani kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Trump kuhusu Ukraine na mambo ya ushuru

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 21, 2025

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa (katikati), Rais Mteule wa Marekani Donald Trump (wakati huo, upande wa kulia) na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mkutano wao mjini Paris, Ufaransa, Desemba 7, 2024. (Picha na Henri Szwarc/Xinhua)

PARIS - Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa atasafiri kuelekea Marekani kufanya mazungumzo na mwenzake wa Marekani, Donald Trump, kujadili suala la Ukraine na ushuru kutozwa na Marekani, Waziri Mjumbe wa Ufaransa wa Masuala ya Ulaya Benjamin Haddad amethibitisha jana Alhamisi.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Ufaransa LCI, Haddad amesema kwamba Macron tayari alikuwa ameshazungumza na Trump mara mbili wiki hii kuhusu Ukraine.

"Msimamo wetu ni kudumisha mazungumzo na rais wa Marekani ili kuhakikisha kuwa sauti ya Watu wa Ulaya inasikika katika majadiliano haya," amesema.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa (Kulia) akikutana na Rais mteule wa Marekani Donald Trump (wakati huo) katika Ikulu ya Elysee mjini Paris, Ufaransa, Desemba 7, 2024. (Xinhua/Gao Jing)

Macron anatarajiwa kusisitiza kwa Trump kwamba "mustakabali wa Ukraine hauwezi kuamuliwa bila Waukraine, na mustakabali na usalama wa Ulaya hauwezi kujadiliwa na kuamuliwa bila Watu wa Ulaya."

Haddad amesisitiza kuwa Ulaya imetoa mchango mkubwa zaidi kwa Ukraine kuliko Marekani, na kwa hiyo, lazima iwe na sauti katika mchakato huo.

Aidha, Macron pia atazungumzia suala la ushuru ambao Trump anapanga kuweka kwa bidhaa za Ulaya. "Vita vya kibiashara, kujihami hakuko kwa maslahi ya yeyote," waziri huyo ameonya.

Wiki hii, Rais Macron aliandaa mkutano wa washirika wa Ulaya na wasio wa Ulaya mara mbili ili kuratibu msimamo wa pamoja kuhusu Ukraine. Mikutano yote hiyo miwili ilihitimishwa kwa msimamo mmoja kwamba mazungumzo yoyote ya amani yanapaswa kushirikisha Ukraine na Ulaya.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha