Wang Yi ahimiza G20 kufanya kazi kama nguvu ya kulinda amani na utulivu duniani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 21, 2025

JOHANNESBURG - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi jana Alhamisi alipotoa hotuba kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Kundi la 20 (G20) uliofanyika Johannesburg nchini Afrika Kusini alitoa wito kwa G20 kufanya kazi kama nguvu ya kulinda amani na utulivu duniani.

“Wakati mawaziri wa mambo ya nje wa G20 wanapokusanyika hapa leo, ni muhimu kurejelea makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa Rio de Janeiro, kufanya kazi pamoja kama nguvu ya kulinda amani na utulivu duniani, na kujenga dunia yenye usalama zaidi,” Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), amesema, akibainisha kuwa China inapenda kushirikiana na pande zote kuelekea lengo hilo.

"Kwanza, tunapaswa kufanya kazi pamoja kama nguvu ya kulinda amani ya dunia," amesema Wang akisisitiza kuwa nchi zote zinapaswa kuheshimu mamlaka na ukamilifu wa ardhi ya kila mmoja vilevile machaguo yao ya njia ya maendeleo na mfumo wa kijamii.

"Pili, tunapaswa kufanya kazi pamoja kama nguvu ya kulinda usalama wa dunia," Wang amesema, akieleza kuwa binadamu ni jumuiya yenye mustakabali wa pamoja na jumuiya ya usalama isiyo na mbadala.

"Tatu, tunapaswa kufanya kazi pamoja kama nguvu ya kutetea mfumo wa pande nyingi," Wang amesema, akibainisha kuwa mwaka huu ni mwaka wa 80 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa na ushindi katika Vita vya Dunia vya Kupambana na Ufashisti.

Akizungumzia mgogoro wa Ukraine, waziri huyo amesema kuwa dirisha la amani linafunguliwa, akisisitiza kwamba China daima inashikilia kutatua mgogoro huo kwa amani mapema na itaendelea kuwa na jukumu la kiujenzi katika utatuzi wake wa kisiasa.

Kuhusu mgogoro wa Gaza, Wang ametoa wito wa kuendelea na utekelezaji mzuri wa makubaliano ya kusimamisha mapigano, na kusisitiza kuwa suluhu ya nchi mbili ndiyo suluhu pekee inayowezekana.

Katika kuhitimisha hotuba yake, Wang amesisitiza kwamba mwaka huu ni "wakati wa Afrika" wa G20, kwani mkutano wa kilele wa G20 utafanyika katika Bara la Afrika kwa mara ya kwanza tangu Umoja wa Afrika uwe mwanachama kamili.

“Tunapaswa kusikiliza sauti ya Afrika, kutilia maana masuala yake inayojali zaidi, kuunga mkono hatua zake, na kufanya juhudi kwa ajili ya amani na maendeleo ya bara hilo,” amesema Wang.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha