

Lugha Nyingine
Rais Putin azungumzia matokeo mazuri ya mazungumzo kati ya Russia na Marekani mjini Riyadh
MOSCOW - Rais Vladimir Putin wa Russia amesema ametaarifiwa kuhusu mazungumzo ya juzi Jumanne kati ya Russia na Marekani mjini Riyadh, akiyaelezea matokeo ya mazungumzo hayo kati ya pande hizo mbili kuwa mazuri, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti jana Jumatano.
"Nimefahamishwa juu ya mazungumzo hayo. Ninayathamini. Kuna matokeo," Putin amesema akijibu maswali ya vyombo vya habari wakati akiwa katika ziara ya kutembelea kiwanda cha kuzalisha UAV mjini St. Petersburg.
Putin amesema amethamini sana matokeo ya mkutano huo wa ngazi ya juu, na kusema majadiliano yamefungua njia kuelekea kuanza tena ushirikiano katika maeneo mbalimbali yanayofuatiliwa na pande zote mbili.
“Mazungumzo kimsingi yalilenga kurejesha uhusiano kati ya Moscow na Washington,” Putin amebainisha, akiongeza kuwa kuimarisha hali ya kuaminiana kati ya nchi zote mbili ni muhimu katika kutatua masuala muhimu, ikiwemo mgogoro wa Ukraine.
“Russia na Marekani zinafanya juhudi pamoja katika masuala muhimu yanayohusiana na ushirikiano wa kiuchumi, anga ya juu na nishati,” amesema.
Rais Putin pia amesema angependa kukutana na Rais wa Marekani Donald Trump, ingawa maandalizi fulani ni muhimu kabla.
Akizungumzia uwezekano wa majadiliano kuhusu Ukraine, Rais Putin amesema Trump alimwambia katika mazungumzo yao kwa njia ya simu kwamba Marekani inaona kwamba Russia na Ukraine zitashirikishwe.
Wajumbe wa Russia na Marekani walifanya mazungumzo juzi Jumanne mjini Riyadh, Saudi Arabia, katika mazungumzo ya kwanza ya ana kwa ana kati ya maafisa waandamizi wa Marekani na Russia tangu kuzuka kwa mgogoro kati ya Russia na Ukraine Februari 2022.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma