Ushuru wa Marekani unaweka "hatari kubwa" kwa uchumi, asema mkuu wa benki kuu ya Ujerumani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 18, 2025

Skrini ikionyesha taarifa za soko la hisa kwenye sakafu ya Soko la Hisa la New York mjini New York, Marekani, Februari 3, 2025. (Picha na Michael Nagle/Xinhua)

FRANKFURT - Mkuu wa Benki Kuu ya Ujerumani, Bundesbank Joachim Nagel, ameonya kwamba ushuru wa Marekani utakuwa na athari mahsusi kwa Ujerumani, ukisababisha "hatari kubwa" kwa ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo.

Akiongea kwenye Hafla ya Maongezi ya Chakula cha Mchana ya Klabu ya Kimataifa ya Umoja mjini Frankfurt jana Jumatatu, Nagel amesisitiza kuwa ikiwa nchi yenye uchumi unaoendeshwa na mauzo ya nje, Ujerumani itapata hasara kubwa kutokana na mabadiliko hayo ya sera ya biashara ya Marekani.

Akirejelea hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump ya kutoza ushuru wa asilimia 25 kwa chuma na aluminiamu, Nagel amebainisha kuwa hatua hiyo itaiathiri hasa Ujerumani, ikisababisha tishio kwa mtazamo wake wa kiuchumi.

Akinukuu makadirio kutoka benki kuu ya Ujerumani, Nagel ameonya kuwa kuongezeka kwa mvutano wa kibiashara katika nchi za Atlantiki kunaweza kusababisha pato la kiuchumi la Ujerumani kwa mwaka 2027 kuwa asilimia 1.5 chini kuliko ilivyotarajiwa. Pia ameonya kuwa mfumuko wa bei unaweza kuongezeka, ingawa athari halisi bado haina uhakika.

Picha hii iliyopigwa Desemba 16, 2024 ikionyesha Jengo la Bunge la Ujerumani, Bundestag mjini Berlin, Ujerumani. (Xinhua/Du Zheyu)

Mkuu huyo wa Benki ya Bundesbank amesisitiza kwamba kuongeza ushuru kutaleta hatari ya kutengeneza "athari za kiuchumi za kujiletea wenyewe" ambazo si tu zinaweza kudhoofisha uchumi wa Ujerumani lakini pia kudhoofisha matarajio ya ukuaji wa uchumi wa Marekani huku ikivuruga minyororo ya usambazaji duniani.

"Mmomonyoko wa uwezo wa kununua na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji kutazidi kwa mbali faida zozote za ushindani kwa viwanda vya Marekani," amesema huku akiongeza kuwa, "Kiwango cha mfumuko wa bei kitaongezeka kwa kasi na kinaweza hata kupanda juu zaidi bila kubanwa sana kwa sera ya fedha."

Kinyume na madai ya serikali Marekani, Nagel amedai kwamba ushuru huo una uwezekano wa kuwa na matokeo mabaya kwa Marekani vilevile.

"Kujihami kiuchumi husababisha hasara kwa ustawi katika nchi zote zilizoathirika. Hakuna washindi," Nagel amehitimisha, akisisitiza dhamira yake katika kutetea mfumo wa biashara ulio wazi na unaozingatia kanuni.

Magari yakionekana kwenye duka la magari ya Volkswagen mjini Berlin, mji mkuu wa Ujerumani, Mei 7, 2020. (Picha na Binh Truong/Xinhua) 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha