Rais Xi Jinping wa China atoa salamu za mwaka mpya wa 2025

(CRI Online) Januari 01, 2025

Katika mkesha wa mwaka mpya, rais Xi Jinping wa China ametoa hotuba ya salamu za mwaka mpya wa 2025 kupitia Shirika Kuu la Utangazaji la China (CMG) na mtandao wa Internet. Ifuatayo ni hotuba hiyo:

Hamjambo! Wakati unapita kwa haraka. Wakati mwaka mpya unawadia, mimi nikiwa hapa Beijing nawatakia kila la heri!

Mwaka 2024, tumepita majira ya machipuko, joto, mpukutiko na baridi kwa pamoja, na pia tumekabiliwa na changamoto na kupata mafanikio kwa pamoja. Mambo mengi yametokea katika mwaka huo usio wa kawaida, na kutuachia hisia na kumbukumbu kubwa.

Tumekabiliana na athari zilizoletwa na mabadiliko ya mazingira ya ndani na ya nje kwa hatua madhubuti, na kutoa sera mbalimbali za “mchanganyiko”, ili kuhimiza kihalisi maendeleo yenye sifa ya juu. Uchumi wa nchi yetu umefufuka na kuwa na mwelekeo mzuri, na pato la taifa kwa mwaka huu linatarajiwa kuzidi renminbi yuan trilioni 130. Uzalishaji wa chakula umezidi tani milioni 700, na tumezalisha chakula zaidi kwa ajili ya watu wetu kuliko zamani. Tumeratibu maendeleo ya sehemu tofauti, na kupata mafanikio makubwa kufuatia msingi mzuri wa awali. Tumeendeleza miji huku tukistawisha vijiji, ili kuhimiza maendeleo ya pamoja. Aidha, tumehimiza kwa kina zaidi maendeleo yasiyoleta uchafuzi kwa mazingira, ili kufanya nchi yetu iwe nzuri zaidi.

Tumekuza tija mpya kufuatia hali yetu maalum, na sasa sekta mpya za kiviwanda zimejitokeza kwa wingi. Mwaka huu tumezalisha magari ya nishati mpya milioni 10 kwa mara ya kwanza, na kupiga hatua mpya katika sekta za mzunguko jumuishi (IC), akili bandia, na mawasiliano ya quantum. Chombo cha Chang’e No. 6 kilichukua sampuli kwenye upande wa mbali wa mwezi kwa mara ya kwanza katika historia ya binadamu. Meli ya utafiti wa kisayansi Mengxiang ilichunguza siri baharini. Barabara yenye kilomita 24 ya kuvuka bahari imeunganisha miji ya Shenzhen na Zhongshan. Kituo cha Qinling kimejengwa barani Antactica. Hayo yote yanaonesha nia ya Wachina katika kutimiza malengo yao makubwa.

Mwaka huu, nilipotembelea maeneo mbalimbali, niliona watu wanaishi maisha bora. Matufaha ya Huaniu kutoka mji wa Tianshui yamekuwa makubwa na mekundu, na meli katika kijiji cha Aojiao, wilayani Dongshan zimejaa samaki. Sanamu yenye “Tabasamu la Mashariki” iliyopo kwenye Mapango ya Maijishan limekuwepo kwa zaidi ya miaka elfu moja, huku utamaduni wa ujirani mwema wa Liuchixiang ukirithishwa kizazi baada ya kizazi. Mtaa wa kiutamaduni wa kale mjini Tianjin umejaa watu wengi, na wakazi wa makabila mbalimbali tofauti mjini Yinchuan wanaishi kama familia moja. Nimefuatilia kwa karibu masuala yanayohusu wananchi kama ajira, kipato, wazee na watoto, elimu na huduma za afya. Katika mwaka huu unaopita, pensheni ya kimsingi imeongezeka, viwango vya riba ya mikopo ya nyumba vimepungua, maeneo yanayofungiwa mahesabu ya bima moja kwa moja yamepanuliwa ili kurahisisha watu wanaokwenda nje ya mikoa kupewa matibabu, na utaratibu wa kubadilisha bidhaa za matumizi za zamani kuwa za mpya umeboresha maisha ya watu… hisia ya kuridhika miongoni mwa watu imeongezeka kwa kiasi kikubwa.

Katika Michezo ya Olimpiki ya Paris, wachezaji wa nchi yetu walijitahidi kwa bidii na kupata matokeo mazuri zaidi katika michezo iliyofanyika nje ya nchi, wakionyesha ari ya kizazi kipya yenye matumaini na kujiamini. Majeshi ya maji na anga yalisherehekea miaka 75 tangu kuanzishwa kwao, na wanajeshi wameonyesha sura mpya. Katika kukabiliana na mafuriko, kimbunga na majanga mengine ya asili, wanachama wengi wa Chama cha Kikomunisti cha China wamejitokeza katika mstari wa mbele, na sote tumeungana na kusaidiana. Wafanyakazi, wajenzi, na wajasiriamali mbalimbali wamejitahidi kufanikisha ndoto zao. Niliwapa tuzo watu waliopewa nishani na heshima za kitaifa, heshima ni kwao, na pia ni kwa kila mmoja anayebeba majukumu kwa uthabiti na anayejitahidi kwa bidii.

Hivi sasa wakati dunia inapokabiliwa na mabadiliko na vurugu mbalimbali, China ikiwa nchi kubwa inayowajibika, imekuwa ikihimiza kikamilifu mageuzi ya usimamizi wa dunia na ushirikiano kati ya nchi za Dunia ya Kusini. Tumesukuma mbele kwa kina zaidi ujenzi wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” kwenye kiwango cha juu, kufanya kwa mafanikio Mkutano wa Kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) mjini Beijing, kufafanua wazi mapendekezo ya China katika mikutano mbalimbali ikiwemo Mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO), Mkutano wa nchi za BRICS, mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Asia Pasifiki (APEC) na mkutano wa G20, na kuingiza msukumo chanya zaidi katika kulinda amani na utulivu duniani.

Tulisherehekea kwa shangwe Maadhimisho ya Miaka ya 75 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, na tukaguswa sana wakati tukikumbuka mabadiliko makubwa yaliyopatikana katika nchi yetu. Katika historia ya zaidi ya miaka elfu tano ya ustaarabu wa taifa letu la China, neno China si kama tu liliandikwa chini ya “He Zun”, chombo kitakatifu cha shaba nyeusi cha kubeba divai na cha kufanyia tambiko cha enzi ya Xizhou, bali pia linakumbukwa daima moyoni mwa kila mtu wa China. Kufanyika kwa Mkutano wa tatu wa wajumbe wote wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kumetoa wito wa kufunga safari ya kukuza mageuzi kwa pande zote. Tukisonga mbele kufuata mwenendo wa zama wa mageuzi na ufunguaji mlango, hakika ujenzi wa mambo ya kisasa wenye umaalum wa China utakuwa na mustakabali mzuri zaidi katika mchakato wa mageuzi na ufunguaji mlango.

Mwaka 2025 tutakamilisha kikamilifu Mpango wa 14 wa Miaka Mitano. Tunatakiwa kutekeleza sera zinazoweza kuchochea hamasa na zenye ufanisi zaidi, kuweka mkazo katika kukuza maendeleo yenye sifa bora, kuhimiza sayansi na teknolojia zenye kiwango cha juu kujiimarisha kwa njia ya kujitegemea na kudumisha mwelekeo mzuri wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Hivi sasa ukuaji wa uchumi unakabiliwa na matatizo mapya, kutoka changamoto zilizoletwa na hali ya sintofahamu ya mazingira ya nje, hadi shinikizo la msukumo wa zamani kubadilishwa kuwa mpya, lakini taabu hizo zote zitaweza kuondolewa kupitia juhudi zetu. Kama tulivyofanya zamani, siku zote tunakua katika kukabiliana na upepo na mvua, na kujiendeleza na kuwa na nguvu zaidi kwa kupita hali ya dhiki. Lazima tujiamini.

Kati ya mambo yote ya familia, ya taifa na ya dunia, jambo muhimu la kwanza ni kuwawezesha wananchi kuishi maisha ya furaha. Kila familia hutumai watoto wao wapate elimu nzuri, wazee wapate huduma nzuri za matunzo, na vijana wapate fursa nyingi zaidi za kujiendeleza. Matumaini haya ndiyo matarajio yao ya kuwa na maisha bora. Tunapaswa kufanya juhudi kwa pamoja, kuendelea kuinua kiwango cha ujenzi na usimamizi wa jamii, kuendelea kujenga mazingira shirikishi yenye masikilizano, kutatua vyema kero na matatizo ya wananchi, ili wawe na tabasamu zaidi usoni na faraja zaidi moyoni.

Katika wakati ambapo China inaadhimisha miaka 25 tangu Macao irejee nyumbani, nilitembelea tena kandoni ya mto Haojiang, na kuona maendeleo na mabadiliko mapya yanayofurahisha. Tutatekeleza kithabiti mkakati wa Nchi Moja, Mifumo Miwili, na kudumisha ustawi na utulivu wa Hongkong na Macao. Ndugu wa kando mbili wote ni wanafamilia, hakuna yeyote anayeweza kukata undugu wetu ulioko katika damu yetu, na wala hakuna yeyote anayeweza kuzuia mkondo mkuu wa kihistoria wa kutimiza Muungano wa Taifa!

Mabadiliko ya dunia ambayo hayakushuhudiwa katika miaka 100 iliyopita yanashika kasi, tunahitaji kuvuka utengano na mgogoro kwa moyo mpana, na kujali mustakabali wa binadamu kwa upendo mkubwa. China inapenda kushirikiana na nchi zote duniani, kuwa watekelezaji wa ushirikiano wa kirafiki, wahimizaji wa kufundishana kwa ustaarabu mbalimbali na washiriki wa ujenzi wa Jumuiya ya Binadamu yenye mustakabali wa Pamoja, na kufungua kwa pamoja mustakbali mzuri wa dunia.

Ndoto ya mbali hutimizwa kwa juhudi endelevu; matumaini magumu hufikiwa kwa dhamira thabiti. Katika safari mpya ya China kuelekea kuwa nchi ya kisasa, kila mmoja ni mhusika mkuu, kila mchango una thamani kubwa, na kila mwanga unang’ara!

Mito na milima vinazidi kuwa tukufu, huku nyota zikiangaza familia zote. Tukaribishe mwaka mpya kwa matumaini mema. Nalitakia taifa letu utulivu, neema na ustawi! Nawatakia ninyi nyote kila la heri, furaha na amani!

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha