Idadi ya watumiaji wa 5G nchini China yafikia zaidi ya bilioni 1

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 24, 2024
Idadi ya watumiaji wa 5G nchini China yafikia zaidi ya bilioni 1
Watu wakitembelea banda la Kampuni ya Mawasiliano ya China Telecom kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Magari ya Kisasa Mwaka 2024 mjini Beijing, mji mkuu wa China, Oktoba 17, 2024. (Xinhua/Chen Zhonghao)

BEIJING – Idadi watumiaji wa huduma za 5G kupitia simu za mkononi imefikia bilioni 1.002 hadi mwisho wa Novemba, ikiwa ni mafanikio makubwa katika nchi hiyo yenye soko kubwa la mawasiliano ya simu za mkononi duniani, takwimu zilizotolewa jana na Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Habari ya China (MIIT) zimeonyesha.

Idadi hiyo inachukua asilimia 56 ya idadi yote ya watumiaji wa simu za mkononi nchini humo, ambayo ni ongezeko la asilimia 9.4 ikilinganishwa na mwisho wa mwaka uliopita.

Ukuaji huo wa kasi unatokana na maendeleo makubwa ya miundombinu. Takwimu hizo za MIIT zinaonyesha kuwa China ilikuwa imeanzisha vituo vya msingi takriban milioni 4.2 vya 5G kufikia mwisho wa mwezi uliopita.

Mapema mwaka huu, hesabu za tasnia hiyo zilionyesha kuwa vituo vya msingi vya 5G vya China -- sehemu ya mawasiliano ya huduma kati ya simu za mkononi na intaneti kubwa – vilichukua asilimia zaidi ya 60 ya jumla ya Dunia, ikionyesha nafasi ya uongozi ya nchi hiyo katika utumiaji wa 5G duniani.

China ina vituo 29 vya 5G kwa kila watu 10,000, ikionyesha kukamilika kwa lengo la maendeleo lililowekwa kwa kipindi cha Mpango wa 14 wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa (2021-2025) kabla ya wakati uliopangwa, alisema Zhang Yunming, naibu waziri wa MIIT, mapema mwezi huu.

Zhang alisema mitandao ya 5G sasa inatoa ufikiaji wa pande zote kote China, ikijumuisha maeneo muhimu kama vile vituo vya huduma za serikali, maeneo ya kitamaduni na utalii, na njia kuu za usafirishaji. Wizara hiyo pia inapanua ufikiaji wa 5G katika maeneo ya vijijini na ya mbali.

MIIT na idara nyingine 11 za serikali kwa pamoja zimetoa mpango uliohuishwa wa matumizi ya kiwango kikubwa ya 5G, ukilenga utekelezaji mkubwa kufikia mwisho wa mwaka 2027.

Ripoti ya tasnia hiyo inakadiria kuwa katika miaka mitano tangu kuzinduliwa kwa huduma ya 5G nchini China mwaka 2019, imehimiza moja kwa moja pato la jumla la kiuchumi la yuan trilioni 5.6 (dola za Kimarekani kama bilioni 767) na kuongeza pato kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwa karibu yuan trilioni 14.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha