Rais Xi Jinping atoa pongezi kwa Siku ya Kimataifa ya kuunga mkono Watu wa Palestina

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 28, 2024

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping ametuma pongezi kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa uliofanyika Jumanne ya Siku ya Kimataifa ya kuunga mkono Watu wa Palestina.

Rais Xi amesema kuwa suala la Palestina ni kiini cha suala la Mashariki ya Kati na linahusu haki na usawa wa kimataifa, kazi kubwa kwa hivi sasa ni kutekeleza kwa pande zote na kwa ufanisi maazimio husika ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kumaliza vita haraka iwezekanavyo na kupunguza hali wasiwasi ya kikanda.

Njia ya kimsingi ni kutekeleza suluhu ya Nchi Mbili na kuhimiza utatuzi wa kisiasa wa suala la Palestina, kuanzisha nchi huru ya Palestina yenye mamlaka kamili kwenye msingi wa mipaka iliyowekwa Mwaka 1967 huku Jerusalem Mashariki ikiwa mji mkuu wake, na kuhakikisha hadhi ya nchi ya watu wa Palestina, haki yao ya kuishi na haki yao ya kurudi kwenye ardhi yao ya awali , Rais Xi amesema.

Amesisitiza kuwa China siku zote inaunga mkono kithabiti mapambano ya haki ya watu wa Palestina ya kurejesha haki zao halali za kitaifa, na inaunga mkono tangu mwanzo mpaka mwisho makundi yote ya Palestina kuimarisha mshikamano na kutekeleza Azimio la Beijing la Kukomesha mafarakano na Kuimarisha Umoja wa Kitaifa wa Palestina ili kufikia upatanisho wa ndani.

“China inaunga mkono kithabiti Palestina kuwa nchi mwanachama rasmi wa Umoja wa Mataifa, na inaunga mkono kuitisha mkutano wa kimataifa wa amani wenye msingi mpana zaidi, wenye maamuzi na heshima zaidi na wenye ufanisi zaidi,” ameongeza Rais Xi.

Amesema China itaendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika kumaliza vita na kukomesha mauaji, kuunga mkono Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina katika Mashariki ya Karibu ili kuendelea kutoa msaada wa huduma za kibinadamu kwa watu wa Gaza, na kuwezesha suala la Palestina kurudi kwenye njia sahihi ya suluhu ya Nchi Mbili ili kufikia mapema zaidi ufumbuzi wa pande zote, wa haki na wa kudumu.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha