Wataalamu wa Kimataifa wakutana nchini Kenya ili kuhimiza kilimo cha mkataba barani Afrika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 13, 2024

NAIROBI – Mkutano wa kimataifa kuhusu kilimo cha mkataba barani Afrika umeanza Jumanne mjini Nairobi, mji mkuu wa Kenya, ukitoa jukwaa kwa wataalam wa kimataifa kujadili njia za kuimarisha ufanisi na ujumuishaji wa kilimo cha mkataba katika bara hilo.

Mkutano huo wa siku mbili umekutanisha washiriki zaidi ya 200, wakiwemo maafisa wa Umoja wa Mataifa, wawakilishi waandammizi wa serikali, wataalam wa sekta hiyo, na wakulima kutoka kote barani Afrika.

Lan Li, mchumi katika Kitengo cha Uchumi na Sera ya Kilimo cha Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, amesema kuwa kilimo cha mkataba kinaweza kutumika kama chombo cha kupitisha viwango rafiki kwa mazingira, kwani makubaliano yanaweza kujumuisha matumizi ya kilimo cha kisasa kinachotilia maanani tabianchi ili kusaidia kupunguza utoaji wa hewa chafu.

“Kilimo cha mkataba ni moja ya nyenzo zinazoweza kusaidia kurasimisha kilimo barani Afrika kwa kufanya kilimo kuwa cha kibiashara na kuongeza tija,” mchumi huyo amesema, akiongeza kuwa kilimo cha mkataba kimeenea katika sekta ya mauzo ya nje, ambapo juhudi ziko juu zaidi kuhakikisha upatikanaji na ubora thabiti.

Erick Ogumo, mtaalamu wa kilimo katika Shirika la Fedha la Kimataifa, amekisema kilimo cha mkataba ni mtindo mmoja wa mageuzi katika kukabiliana na baadhi ya changamoto zinazokabili sekta ya kilimo barani Afrika.

Kwa mujibu wa Ogumo, mtindo huo unanufaisha wakulima na wanunuzi kwa kuwapa wakulima masoko ya uhakika ya mazao yao huku ukiwapa wanunuzi ufikiaji thabiti wa bidhaa zenye ubora wa juu.

Hata hivyo, Ogumo amesisitiza kuwa Afrika lazima itekeleze sera na mifumo ya kisheria ili kufungua kikamilifu uwezo wa kilimo cha mkataba na kulinda pande zote zinazohusika.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha