Rais Xi wa China aagiza juhudi zote kutibu majeruhi wa tukio la makumi ya watu kugongwa kwa gari mjini Zhuhai, Guangdong

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 13, 2024

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping ameagiza kufanya juhudi zote za kutibu majeruhi katika tukio la dereva kuendesha gari kugonga makumi ya watu siku ya Jumatatu katika Mji wa Zhuhai, Mkoa wa Guangdong, Kusini mwa China.

Katika maagizo kuhusu tukio husika, Rais Xi, ambaye pia ni katibu mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kijeshi ya China (CMC), ametaka mhusika aadhibiwe vikali kwa mujibu wa sheria.

Tukio hilo lilitokea katika kituo cha michezo mjini Zhuhai, likisababisha vifo vya watu 35 na wengine 43 kujeruhiwa vibaya.

Rais Xi amezitaka serikali zote za mitaa na mamlaka husika kupata mafunzo kutokana na tukio hilo, na kuimarisha kazi ya kuzuia na kudhibiti chanzo cha hatari.

Pia amesisitiza umuhimu wa kusuluhisha mizozo kwa wakati, kuzuia kutokea kwa matukio yenye kuleta hali mbaya kabisa, na kufanya kila juhudi kulinda usalama wa maisha ya watu na utulivu wa jamii.

Waziri Mkuu wa China Li Qiang amezitaka idara husika kushughulikia ipasavyo madhara ya tukio hilo, kuchunguza haraka tukio hilo na kuadhibu vikali mhusika kwa mujibu wa sheria.

Li, ambaye pia ni mjumbe wa kudumu wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya CPC, amehimiza juhudi za kupanga mpango wa jumla wa kuzuia na kudhibiti hatari ili kuhakikisha utulivu wa jamii.

Kufuatia maagizo ya Rais Xi, serikali kuu ya China imetuma kikundi cha kuelekeza kazi ya kushughulikia tukio hilo. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha