Waziri wa mambo ya nje wa China afanya mazungumzo na mwenzake wa Korea Kusini

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 14, 2024

BEIJING - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amefanya mazungumzo na Cho Tae-yul, waziri wa mambo ya nje wa Korea Kusini, mjini Beijing siku ya Jumatatu ambapo amesema kuwa China na Korea Kusini ni majirani wa karibu na zinapaswa kudumisha mawasiliano ya mara kwa mara.

"Hivi karibuni, uhusiano kati ya China na Korea Kusini umekuwa ukikabiliwa na matatizo na changamoto, jambo ambalo haliendani na maslahi ya pamoja ya pande hizo mbili, wala si jambo ambalo China inataka kuona," amesema Wang huku akiongeza kuwa ni matumaini kuwa Korea Kusini itashirikiana na China kushikamana na nia ya awali ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia, kufuata mwelekeo wa ujirani mwema na urafiki, kushikilia lengo la ushirikiano wa kunufaishana, kuondoa misukosuko na kufanya juhudi kwa pamoja kusukuma mbele maendeleo mazuri na tulivu ya uhusiano kati ya China na Korea Kusini.

Wang, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), amebainisha kuwa China na Korea Kusini zinapaswa kuelewana na kuheshimiana, kuimarisha mawasiliano, kuondoa sintofahamu na kuimarisha hali ya kuaminiana.

Wang ameongeza kuwa, China inatumai Korea Kusini utafuata kanuni ya kuwepo kwa China moja, kushughulikia ipasavyo na kwa busara masuala yanayohusiana na Taiwan, na kuimarisha msingi wa kisiasa wa uhusiano kati ya pande mbili.

Kwa upande wakle Cho Tae-yul amesema kuwa, anatumai ziara yake hiyo nchini China itakuwa hatua muhimu ya kusonga mbele katika uhusiano kati ya Korea Kusini na China na kwamba serikali ya Korea Kusini inatilia maanani sana uhusiano kati yake na China, na inatarajia kushirikiana kwa karibu na China ili kuendeleza ushirikiano wa kimkakati na kiwenzi ulio mzuri na uliokomaa zaidi juu ya misingi ya kuheshimiana, kutendeana kwa usawa na maslahi ya pamoja.

Pande hizo mbili pia zimebadilishana maoni kuhusu ushirikiano kati ya China-Japan-Korea Kusini, hali ya Peninsula ya Korea na masuala mengine yanayofuatiliwa kwa pamoja.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha