Afrika yaharakisha maendeleo ya nishati mbadala

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 10, 2024

Ripoti husika kutoka Shirika la Kimataifa la Nishati inasema kuwa Afrika ina rasilimali nyingi za nishati mbadala na ina uwezo mkubwa wa kuendeleza nishati mbadala. Katika miaka ya hivi karibuni, nchi za Afrika zimeharakisha maendeleo ya nishati mbadala. China inatilia maanani sana ushirikiano wa nishati mbadala kati yake na Afrika, na kampuni nyingi zaidi za China zinashiriki katika mchakato wa maendeleo ya kijani barani Afrika.

Kuhimiza ujenzi wa miradi ya nishati mbadala

Hivi sasa, nchi nyingi za Afrika zinafanya juhudi kuhimiza ujenzi wa miradi ya nishati mbadala. Shirika la Taifa la Usimamizi wa Nishati la Tunisia hivi majuzi lilitangaza kuyafanya maendeleo ya nishati mbadala kama mkakati wa taifa hilo na kuweka jitahidi katika kuongeza kiwango cha kuzalisha umeme kwa nishati mbadala kwenye uzalishaji wa jumla wa umeme kutoka chini ya asilimia 3 Mwaka 2022 hadi asilimia 24 ifikapo Mwaka 2025.

Namibia inapanga kuzalisha asilimia 70 ya nishati yake kutoka kwa vyanzo mbadala ifikapo Mwaka 2030. Kenya imetambua miradi ya nishati ya upepo, jotoardhi na nishati nyingine mbadala kama vipaumbele vya maendeleo.

"Ripoti ya Mtazamo wa 2023" iliyotolewa na Shirikisho la Tasnia ya Nishati ya Jua la Afrika mwaka jana ilionyesha kuwa tasnia ya nishati ya jua barani Afrika inaendelezwa kwa kasi. Nchi kama vile Afrika Kusini, Morocco, na Misri zinaendelea kuongoza katika miradi ya ujenzi wa paneli za umeme wa jua. Nchi nyingi zaidi za kanda hii, kama vile Cape Verde, Botswana, na Eritrea, zinaongeza uwekezaji katika tasnia ya nishati ya jua na kuanza kujenga na kuendesha miradi mikubwa ya namna hiyo.

Afrika ina uwezo mkubwa wa kuendeleza nishati mbadala

Katika shughuli ya Wiki ya Maendeleo Endelevu ya Abu Dhabi Mwaka 2023, washiriki walizindua kwa pamoja Mpango wa Maendeleo ya Tasnia ya Nishati Mbadala ya Afrika, wakiamini kwamba Afrika ina nguvu bora ya nishati mbadala na uwezo mkubwa wa maendeleo.

Benki ya Dunia ina matumaini kuhusu mustakabali wa maendeleo ya nishati mbadala barani Afrika na hivi karibuni imekubali kuwekeza dola za Marekani milioni 311 kwenye miradi ya nishati mbadala katika Afrika Magharibi na Kati.

Mwezi Mei, 2022, Muungano wa Hidrojeni ya Kijani wa Afrika, ulioanzishwa na nchi sita za Afrika Kusini, Namibia, Kenya, Misri, Morocco na Mauritania, ulizinduliwa rasmi kwa lengo la kuhamasisha Bara la Afrika kuharakisha uhamiaji wake kutoka kwenye nishati ya mafuta na kuhamia nishati mbadala.

China yatoa msaada kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa "Afrika ya Kijani"

Katika miaka ya hivi karibuni, China imeendelea kuimarisha ushirikiano kati yake na nchi za Afrika katika nyanja za nishati mbadala kama vile nishati za maji, jua, upepo na uhifadhi wa nishati ili kusaidia maendeleo ya tasnia zinazohusiana.

Katika eneo la Kiryandongo lililoko katikati na magharibi mwa Uganda, Kituo cha Kuzalisha Umeme kwa Maji cha Karuma kilichojengwa na Kampuni ya Sinohydro ya China kina uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 600. Baada ya kukamilika, kitakuwa kituo kikubwa zaidi cha kuzalisha umeme kwa nishati safi nchini Uganda.

Kituo cha Kuzalisha Umeme kwa Jua cha Garissa nchini Kenya, kilichojengwa na Kampuni ya Ushirikiano wa Kimataifa wa Uchumi na Teknolojia ya Jiangxi, China kina uwezo wa kuzalisha umeme wa Megawati 50 na ndicho kituo kikubwa zaidi cha kuzalisha umeme kwa jua katika Afrika Mashariki hadi kufikia sasa.

Kituo cha kuzalisha umeme kwa maji cha Lower Kaifuxia kilichojengwa na Kampuni ya Ujenzi wa Nishati ya China kimepunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa umeme nchini Zambia na kuharakisha maendeleo ya uchumi ya Zambia na hata nchi za Kusini mwa Afrika.

Mkurugenzi wa Kituo cha Masomo Kuhusu China katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nchini Tanzania, Humphrey Moshi amemwambia mwandishi wa makala hii kuwa teknolojia ya nishati mbadala ya China ina gharama nafuu, inafaa kwa mazingira ya Afrika na hali nzuri ya kuunganisha.

Amesema, kuimarisha ushirikiano wa Afrika na China katika nishati mbadala, kutasaidia kuongeza uwezo wa maendeleo endelevu wa Afrika, na pia kusaidia Afrika kuziba pengo la uhaba wa kiufundi katika sekta husika.

Kupitia ushirikiano wa mara kwa mara, nchi za Afrika zimejifunza teknolojia ya hali ya juu na uzoefu wa usimamizi wa China. "Tunatarajia Afrika na China kuhimiza zaidi ushirikiano katika nishati mbadala, kuendelea kuimarisha miundo na msingi wa ushirikiano, na kusaidia kutekeleza mpango wa 'Afrika ya Kijani'," Moshi amesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha