

Lugha Nyingine
Kampuni ya magari ya BYD ya China yaongoza duniani kwa kuuza magari yanayotumia umeme katika Robo ya 4 ya Mwaka 2023
Gari la milioni tano la nishati mpya (NEV) kutengenezwa na kampuni ya BYD ya China likitoka kwenye mstari wa uzalishaji wa kiwanda mjini Shenzhen, Mkoa wa Guangdong, Kusini mwa China, Agosti 9, 2023. (Xinhua/Liang Xu)
SHENZHEN – Kampuni ya magari ya BYD ya China imekuwa muuzaji anayeongoza duniani wa magari yanayotumia nishati ya umeme kikamilifu katika robo ya nne ya Mwaka 2023, ikiashiria hatua nyingine ya kihistoria kwa tasnia ya magari yanayotumia nishati mpya (NEV) ya China inayokua kwa kasi ambapo kampuni hiyo ya magari yenye makao yake makuu mjini Shenzhen imetangaza kuwa magari 526,409 yanayotumia umeme kikamilifu yameuzwa kati ya Oktoba na Desemba mwaka 2023, ikiipita idadi ya magari 484,507 ya Kampuni ya magari ya Tesla ya Marekani katika kipindi kama hicho.
Takwimu hizo za kila mwaka pia zimeshuhudia BYD ikidumisha nafasi yake ya kuwa muuzaji mkuu wa NEV duniani, huku magari zaidi ya milioni 3.02 yakiuzwa mwaka jana, ikiwa ni pamoja na modeli zinazotumia umeme kikamilifu na zile za nishati mchanganyiko.
BYD ni moja ya wazalishaji wengi wa NEV ambao wameshuhudia mauzo yakiongezeka wakati ambapo China ikijivunia idadi kubwa zaidi ya magari duniani na kuelekea teknolojia za kijani.
Kampuni nyingine za China zilizochomoza na takwimu zao za mauzo ni pamoja na GAC Aion (480,000) na Li Auto (376,000) wakati kampuni kubwa ya NEV ya Tesla ya Marekani pia imefurahia ukuaji wa asilimia 38 katika uuzaji wa magari hayo Mwaka 2023.
Ikiwa ilianzishwa Mwaka 1995 kama mzalishaji wa betri, Kampuni ya BYD ilikuwa mwanzilishi wa mapema katika juhudi za kutengeneza magari ya NEV nchini China. Mwaka 2004, wakati magari yanayotumia nishati mpya ya BYD yalipoonyeshwa kwa mara ya kwanza kwenye maonyesho ya kimataifa ya magari ya Beijing, kampuni hiyo ndiyo ilikuwa mtengenezaji pekee aliyeonyesha NEVs.
"Tulipotangaza kwa mara ya kwanza mpango wetu wa utengenezaji wa gari linalotumia nishati ya umeme, siyo watu wengi waliokuwa na imani nasi," amesema Wang Chuanfu, Mwenyekiti wa BYD.
"Lakini tulikuwa na imani katika utabiri wetu kwamba soko la magari ya kawaida litakuwa na kikomo cha juu kutokana na mazingira na mabadiliko ya tabianchi," Wang amesema.
Watembeleaji wakipata maelezo kuhusu magari yanayotumia nishati mpya ya Kampuni ya magari ya BYD ya China kwenye Maonyesho ya 27 ya Magari ya Kimataifa ya Eneo la Ghuba Kuu ya Guangdong-Hong Kong-Macao katika Kituo cha Mikutano na Maonyesho cha Shenzhen mjini Shenzhen, Mkoa wa Guangdong, Kusini mwa China, Juni 16, 2023. (Xinhua/Liang Xu)
Picha hii iliyopigwa Oktoba 17, 2023 ikionyesha magari yanayotumia nishati mpya yakichajiwa kwenye eneo la kuchaji katika Mji mdogo wa Gujiao ulioko Eneo linalojiendesha la Makabila ya Wabouyei na Wamiao la Qiannan, Mkoa wa Guizhou, Kusini-Magharibi mwa China. (Xinhua/Tao Liang)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma