

Lugha Nyingine
ECOWAS yaanzisha kituo cha taarifa ili kuimarisha uratibu wa usambazaji wa umeme
Picha hii iliyopigwa Novemba 17, 2023 ikionyesha Kituo cha Taarifa na Uratibu cha West African Power Pool (WAPP) cha Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) huko Abomey Calavi, Benin. (Picha na Seraphin Zounyekpe/Xinhua)
COTONOU, Benin - Kituo cha Taarifa na Uratibu cha kuchangia nishati cha Afrika Magharibi (West African Power Pool, WAPP) cha Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) kimezinduliwa siku ya Ijumaa huko Abomey Calavi, mji ulioko Kusini mwa Benin ambapo kinalenga kuongeza na kuendeleza miundombinu ya uzalishaji na usambazaji wa umeme, na kuratibu mabadilishano ya umeme kati ya nchi wanachama wa ECOWAS.
Pia ni jukwaa la kuratibu uendeshaji wa WAPP, ambalo litawezesha gridi za taifa za umeme kuunganishwa katika soko la umeme la kikanda, ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa bei ya nafuu kwa watu wa nchi wanachama wa ECOWAS kwa makubaliano ya muda wa kati na mrefu.
Mtandao huu uliounganishwa utawezesha mauzo na manunuzi ya umeme kuanzia robo ya kwanza ya Mwaka 2024, bila kujali eneo la kijiografia katika kanda hiyo, amesema Damtien L. Tchintchibidja, Makamu wa Rais wa Kamisheni ya ECOWAS.
"Ni asilimia 52 tu ya wakazi wote wa Afrika Magharibi ndiyo wanaopata umeme kwa sasa. Kwa wale wanaopata huduma hiyo, uhakika wa upatikanaji wa umeme bado ni changamoto kubwa: kukatika umeme kwa muda mrefu, kukatika kwa umeme bila kutarajiwa, uharibifu wa vifaa vya nyumbani na vifaa vya umeme ni tatizo lao la kila siku." amesema Kwawu Mensan Gaba, meneja wa utendaji wa Benki ya Dunia.
Utaratibu wa kuchangia nishati wa Afrika Magharibi WAPP, iliyoundwa kwa uamuzi wa wakuu wa nchi na serikali katika Mkutano wa 29 wa ECOWAS, umeshaunganisha nchi 14 kati ya nchi wanachama 15 wa jumuiya hiyo ya kiuchumi ya kikanda.
Mfanyakazi akifanya kazi kwenye Kituo cha Taarifa na Uratibu cha West African Power Pool (WAPP) cha Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) huko Abomey Calavi, Benin, Novemba 17, 2023. (Picha na Seraphin Zounyekpe/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma