China kuendeleza uvumbuzi, kufungua mlango na kutoa fursa zaidi kwa Dunia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 09, 2023

Makamu wa Rais wa China Han Zheng akitoa hotuba kuu kwenye hafla ya ufunguzi wa Baraza la sita la Uchumi la Bloomberg nchini Singapore, Novemba 8, 2023. (Xinhua/Gao Jie)

Makamu wa Rais wa China Han Zheng akitoa hotuba kuu kwenye hafla ya ufunguzi wa Baraza la sita la Uchumi la Bloomberg nchini Singapore, Novemba 8, 2023. (Xinhua/Gao Jie)

SINGAPORE - Makamu wa Rais wa China, Han Zheng, amesema Jumatano wakati akitoa hotuba yake kuu kwenye Baraza la sita la Uchumi Mpya la Bloomberg lililofanyika nchini Singapore, kwamba China itaendelea kuhimiza uvumbuzi ili kuendesha uchumi wa Dunia, kutafuta ushirikiano kupitia kufungua mlango, na kutoa fursa zaidi za soko na uwekezaji duniani kote.

"China itaendeleza bila kuyumbayumba kiwango cha juu cha ufunguaji mlango kwa nchi za nje, na iko tayari kutoa fursa zaidi za soko na uwekezaji ili kunufaishana faida za ufunguaji mlango na kampuni za dunia," Han amesema.

Amebainisha kuwa China itaendelea kuleta maendeleo zaidi kupitia uvumbuzi ambao ndiyo msukumo wa uchumi wa dunia katika kuharakisha ongezeko la uchumi na kusonga mbele kwa kasi.

Amesema China iko tayari kushirikiana na nchi nyingine kudumisha amani na usalama duniani, kutafuta maendeleo ya pamoja na ustawi wa nchi zote, na kujenga jumuiya yenye mustakabali wa pamoja wa binadamu.

Kuhusu uhusiano kati ya China na Marekani, Han amesema kuwa mawasiliano muhimu ya hivi karibuni ya ngazi ya juu kati ya China na Marekani yameongeza matarajio chanya ya jumuiya ya kimataifa kwa ajili ya kuboreshwa kwa uhusiano kati ya China na Marekani katika siku zijazo.

“China iko tayari kuimarisha mawasiliano na mazungumzo na Marekani, kuhimiza ushirikiano wa kunufaishana, kudhibiti ipasavyo tofauti kati ya nchi hizo mbili, na kufanya juhudi za pamoja za kutatua changamoto za kimataifa,” amesema Han Zheng huku akitaja masuala kama mabadiliko ya tabianchi na migogoro ya siasa za kijiografia.

Han pia alikutana pembezoni na Mike Bloomberg, mwanzilishi wa Baraza la Uchumi Mpya la Bloomberg na Kampuni ya Bloomberg L.P., na wawakilishi wa wageni waliohudhuria shughuli hiyo.

Katika ziara yake nchini Singapore, Han alikutana na Rais wa Singapore Tharman Shanmugaratnam, Waziri Mkuu Lee Hsien Loong na maafisa wengine waandamizi wa serikali.

Baraza la 6 la Uchumi Mpya la Bloomberg linafanyika hapa Novemba 8-10, na kaulimbi ya mwaka huu inasema "Kukabiliana na Hali ya Ukosefu wa Utulivu." Linaangazia changamoto zinazokabili uchumi wa Dunia na kusisitiza fursa ya kushughulikia masuala ya msingi kama vile mfumuko wa bei unaoendelea, mivutano ya siasa za kijiografia, kuongezeka kwa teknolojia za akili bandia na mabadiliko ya tabianchi.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha