Ripoti mpya yathibitisha rekodi ya juu ya hewa chafu, kuinuka kwa kiwango cha bahari duniani na joto la bahari katika Mwaka 2022

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 07, 2023

Mtu akipiga picha za mawimbi makubwa ya bahari kwenye Fukwe ya Newport, California, Marekani, Agosti 20, 2023. (Xinhua)

Mtu akipiga picha za mawimbi makubwa ya bahari kwenye Fukwe ya Newport, California, Marekani, Agosti 20, 2023. (Xinhua)

LOS ANGELES - Ripoti ya mapitio ya kila mwaka ya tabianchi duniani iliyotolewa mtandaoni Jumatano imesema, uzito wa hewa chafu, kiwango cha bahari duniani na hali joto ya bahari vilifikia kiwango cha juu zaidi Mwaka 2022.

Ripoti ya Hali ya Tabianchi, ambayo ni tathmini ya 33 ya kila mwaka iliyokusanywa na Vituo vya Kitaifa vya Taarifa za Mazingira katika Idara ya Taifa ya Usimamizi wa Bahari na Mazingira Anga ya Marekani, inategemea mchango waliotoa wanasayansi zaidi ya 570 katika zaidi ya nchi 60.

Inatoa taarifa ya kina zaidi iliyohuishwa juu ya viashiria vya tabianchi vya Sayari ya Dunia, matukio muhimu ya hali ya hewa na data nyingine zilizokusanywa na vituo vya ufuatiliaji wa mazingira na vyombo vilivyo kwenye nchi kavu, kwenye maji na barafu na angani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, uzito wa hewa chafu duniani ulikuwa wa kiasi kikubwa zaidi kuwahi kurekodiwa Mwaka 2022. Mwenendo wa ongezeko la joto uliendelea kote duniani.

Uchambuzi mbalimbali wa kisayansi unaonyesha kuwa halijoto ya kila mwaka ya uso wa Dunia ilikuwa nyuzi joto 0.25 hadi 0.30 zaidi ya wastani wa kati ya Mwaka 1991-2020.

Ripoti hiyo imesema, Hali ya baridi kali, La Niña katika ikweta ya Bahari ya Pasifiki ambayo ilianza katikati ya Mwaka 2020, ikiwa na mapumziko mafupi Mwaka 2021, iliendelea hadi mwaka mzima wa 2022.

Mawimbi ya joto yalivunja rekodi za halijoto katika sayari nzima, kwa mujibu wa ripoti hiyo. Mwezi Julai, wimbi la joto kali lililodumu kwa siku 14 lilikumba Ulaya Magharibi.

Joto kali lililovunja rekodi katika majira ya joto katikati na mashariki mwa Bara la Asia, haswa katika bonde la Mto Changjiang, limesababisha ukame mbaya ulioathiri zaidi ya watu milioni 38 na kusababisha hasara ya moja kwa moja ya kiuchumi ya dola bilioni 4.75 za Kimarekani, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Watoto wakipoza joto la mwili kwenye Chemchemi ya Crown katikati mwa jiji la Chicago, Marekani, Agosti 23, 2023. (Picha na Vincent D. Johnson/Xinhua)

Watoto wakipoza joto la mwili kwenye Chemchemi ya Crown katikati mwa jiji la Chicago, Marekani, Agosti 23, 2023. (Picha na Vincent D. Johnson/Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha