

Lugha Nyingine
Kijana wa Tanzania avunja pengo katika elimu, ubunifu wa kidijitali wa afya
Deogratius Mosha, mwanzilishi mwenza wa Kampuni ya Mainstream Media, kampuni iliyoanzishwa Mwaka 2015 inayojishughulisha na ubunifu wa kidijitali na uendelezaji wa program za kiteknolojia, akifanya mahojiano jijini Dar es Salaam, Tanzania, Aprili 18, 2023. (Picha na Herman Emmanuel/Xinhua)
DAR ES SALAAM - Pilika Nwaka Mwamsaku, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Katoliki mkoani Mbeya, Tanzania anaamini kuwa masomo yake yamerahisishwa kwa kutumia ubunifu wa kidijitali uitwao Smart University Initiative, au SmartUni kwa kifupi.
"Kupitia jukwaa la SmartUni, ninapata nyenzo zote za kusomea ninazohitaji baada ya mihadhara. Pia natumia jukwaa hili kubadilishana mawazo na wanafunzi kutoka vyuo vikuu vingine vinavyohusiana na programu hii," Mwamsaku, ambaye anasomea shahada ya usimamizi wa biashara, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua katika mahojiano ya hivi majuzi.
Ameongeza kuwa kupitia SmartUni, wanafunzi wanaweza kupata notisi za masomo kwa kutumia programu hiyo badala ya kutumia fedha kidogo walizo nazo kulipia nakala hizo na kuongeza kuwa programu hiyo hutumika pia kwa ajili ya kuonyesha ratiba za darasani.
Mwamsaku ni miongoni mwa makumi ya maelfu ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Tanzania wanaotumia programu ya SmartUni, shukrani kwa Deogratius Mosha, mwanzilishi mwenza wa Kampuni ya Mainstream Media, kampuni iliyoanzishwa Mwaka 2015 inayojishughulisha na uvumbuzi wa kidijitali na uendelezaji wa program za kiteknolojia.
Akiwa na umri wa miaka 35, Mosha tayari amevunja pengo la kiteknolojia kwa kuvumbua SmartUni, ambayo ni suluhu ya kidijitali inayoweka mfumo wa kidijitali kwenye mfumo wa elimu katika ngazi ya chuo kikuu, suluhu inayolenga kupunguza matumizi ya karatasi na kuchapisha notisi kwa wanafunzi na wahadhiri.
"SmartUni ni suluhu ya kidijitali iliyoundwa kwa ajili ya kubadilisha maisha ya wanafunzi katika vyuo vikuu na vyuo vya kati kwa kuwapa fursa ya kupata nyenzo za kusomea kupitia simu za mkononi na wavuti," Mosha ameliambia Xinhua mjini Dar es Salaam huku akieleza kuwa ubunifu huo aliuanza Julai, 2022.
Mosha amesema ubunifu mwingine alioufanya ni kwenye huduma ya afya ya kidijitali iitwayo Afya Tap, ambayo ni suluhisho linalowaunganisha madaktari, wagonjwa na wahudumu wengine wa afya.
"Ubunifu huu ulianza wakati janga la UVIKO-19 lilipozuka nchini Mwaka 2020. Tuligundua kuwa watu wengi waliogopa kwenda kwenye maduka ya dawa, waliogopa kwenda hospitalini walipopata dalili za UVIKO-19," amesema.
Mosha, ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Kwanza ya Sayansi (Habari na Teknolojia), alishinda Tuzo za Arobaini za Washiriki wenye umri chini ya 40 za Afrika za Mwaka 2022 katika kipengele cha sayansi, teknolojia na uvumbuzi.
Deogratius Mosha, mwanzilishi mwenza wa Kampuni ya Mainstream Media, kampuni iliyoanzishwa Mwaka 2015 inayojishughulisha na ubunifu wa kidijitali na uendelezaji wa program za kiteknolojia, akionyesha programu yake jijini Dar es Salaam, Tanzania, Aprili 18, 2023. (Picha na Herman Emmanuel/Xinhua)
Deogratius Mosha, mwanzilishi mwenza wa Kampuni ya Mainstream Media, kampuni iliyoanzishwa Mwaka 2015 inayojishughulisha na ubunifu wa kidijitali na uendelezaji wa program za kiteknolojia, akionyesha programu yake jijini Dar es Salaam, Tanzania, Aprili 18, 2023. (Picha na Herman Emmanuel/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma