Tanzania yakaribisha uwekezaji kwenye sekta ya TEHAMA na mageuzi ya kidijitali

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 24, 2023

DAR ES SALAAM - Makamu wa Rais wa Tanzania Philip Mpango Alhamisi aliwaalika wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani kuwekeza katika sekta teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) na mageuzi ya kidijitali.

“Mageuzi ya TEHAMA na kidijitali ni miongoni mwa vichocheo muhimu vya maendeleo ya haraka,” amesema Mpango wakati akifungua Jukwaa la kwanza la Biashara kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Amesema sera ya taifa ya TEHAMA nchini Tanzania inahimiza uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu ya kidijitali kama vile maeneo maalumu ya data na taasisi za teknolojia za kidijitali.

"Hatua hii inalenga kuongeza ujuzi na kutumia uvumbuzi wa kidijitali kama vile uhandisi wa roboti na akili bandia," ameliambia jukwaa hilo lililohudhuriwa na zaidi ya wawekezaji 800 kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na zaidi ya makampuni 150 ya Tanzania.

Mpango ameyataja maeneo mengine ya uwekezaji kuwa ni sekta ya kilimo, usafirishaji, utalii, nishati na viwanda.

Amesema Serikali ya Tanzania imejikita katika kujenga uchumi imara unaotegemezwa na mihimili minne ya mageuzi, maridhiano, uhimilivu na kujenga upya.

Pia amesema mageuzi hayo, miongoni mwa mengine, yanalenga kuongeza uwazi, kukabiliana na vizuizi na changamoto nyingine zinazohusiana na biashara na uwekezaji.

“Aidha, Serikali imechukua hatua ya kuimarisha na kufanya utendaji wa kisasa kwenye Kituo cha Uwekezaji cha Tanzania na Mamlaka ya Uhimizaji wa Uwekezaji ya Zanzibar ili ziweze kutumika kikamilifu kama vituo vya uhamasishaji na uwezeshaji wa uwekezaji,” amesema Mpango.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha