

Lugha Nyingine
Wanaanga wa China kwenye chombo cha Shenzhou-15 kufanya matembezi kwenye anga ya juu
Hafla ya kuwaaga wanaanga watatu wa chombo cha anga ya juu cha Shenzhou-15 ikifanyika kwenye Kituo cha Urushaji Satelaiti cha Jiuquan, Kaskazini-Magharibi mwa China, Novemba 29, 2022. (Xinhua/Liu Lei)
BEIJING - Wanaanga wa China kwenye chombo cha Shenzhou-15, ambao kwa sasa wako kwenye kituo cha anga ya juu cha China cha Tiangong, watafanya shughuli zao za kwanza nje ya chombo ndani ya siku chache zijazo, Shirika la Anga za Juu la China limetangaza Jumatano.
Wanaanga hao watatu wamekuwa wakiishi katika obiti kwa siku 70 tangu walipoingia kwenye muunganiko wa kituo cha anga ya juu cha China Novemba 30, 2022. Wamekamilisha kazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kubadilishana kwenye obiti kati ya wanaanga hao na wanaanga wa Shenzhou-14, majaribio ya kupima kabini za majaribio ya kisayansi, na ukaguzi wa vifaa vya anga.
Pia wamefanya upimaji wa afya , mazoezi ya kuzuia uzani na majaribio mfululizo ya sayansi kwenye anga ya juu.
Hata hivyo, miezi miwili iliyopita haikuwa tu kuhusu kazi. Wakaazi hao wapya wa kituo cha anga ya juu cha China pia walisherehekea Mwaka Mpya wa Jadi wa China na kufanya maonyesho ya picha zilizochorwa nao au kupigwa nao kwa kamera kwenye anga ya juu, na kutuma salamu za Mwaka Mpya kwa watu wa China.
Kwa mujibu wa shirika hilo, wanaanga hao watatu wa Shenzhou-15 sasa wako katika hali nzuri, na muunganiko wa kituo cha anga ya juu unaendelea kufanya kazi kwa utulivu. Mazingira yote yamewekwa sawa kwa ajili matembezi ya kwanza nje ya chombo kwenye anga ya juu kwa wanaanga hao.
Wanaanga hao watatu wa Chombo cha Shenzhou-15 ni Fei Junlong, Deng Qingming na Zhang Lu. Majukumu yao ya miezi sita yanalenga kumalizia hatua ya mwisho ya ujenzi wa kituo cha anga ya juu cha China na kuanza hatua ya kwanza ya matumizi na maendeleo yake.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma