

Lugha Nyingine
Uzalishaji wa roboti za viwandani nchini China waongezeka Mwaka 2021
Picha iliyopigwa Agosti 18, 2022 ikionyesha roboti ya viwandani kwenye maonyesho ya Mkutano wa Dunia wa Roboti Mwaka 2022 uliofanyika kuanzia Agosti 18 hadi 21 mjini Beijing. (Xinhua/Zhang Chenlin)
BEIJING - Guo Shougang, Ofisa wa Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Habari ya China amesema Jumanne wiki hii kwamba China ni soko kubwa zaidi duniani la roboti za viwandani, na uzalishaji wake ulifikia roboti 366,000 Mwaka 2021, ikiwa ni ongezeko la mara 10 kutoka Mwaka 2015.
Roboti za viwandani zinatumika katika nyanja 60 za sekta ya viwanda nchini China. Mwaka 2021, utumiaji wa roboti za viwandani ulizidi roboti 300 kwa kila watu 10,000, ikiwa ni kama mara 13 zaidi ya Mwaka 2012.
Roboti za kutoa huduma hutumiwa sana katika nyanja kama vile huduma za chakula, elimu, matibabu na uchukuzi. Kwa mujibu wa mtandao wa kutoa habari za biashara wa Tianyancha, kwa sasa, kuna zaidi ya makampuni 439,000 yanayohusiana na roboti nchini China, kati ya hayo zaidi ya 79,000 ni mapya yaliyosajiliwa kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu.
Kiwango cha kiteknolojia cha sekta ya roboti ya China kimeboreshwa zaidi, amesema Guo, huku akiongeza kuwa maendeleo yamepatikana katika utafiti na uundaji wa vipengele muhimu ikiwa ni pamoja na vipunguza kasi kwa usahihi, vidhibiti vinavyotumia akili bandia na mifumo ya uendeshaji kwa wakati halisi.
Guo amesema, wizara hiyo itaboresha viwango, mifumo ya upimaji na uthibitishaji, kuharakisha juhudi za kuimarisha maeneo dhaifu katika nyenzo maalum, vipengele vya msingi na teknolojia ya usindikaji, kukuza biashara za ubora wa juu, na kuweka mazingira mazuri kwa sekta ya roboti.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma