Wanasayansi wa Uganda waunda mfumo wa ufuatiliaji wa ubora wa hewa wenye gharama nafuu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 16, 2022

Fundi akifanya kazi ndani ya karakana ya AirQo kwenye Chuo Kikuu cha Makerere mjini Kampala, Uganda, Mei 31, 2022. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)

KAMPALA - Katika karakana ndogo iliyopo Chuo Kikuu cha Makerere, nchini Uganda vijana wenye ujuzi wa teknolojia wanaunda mfumo wa ufuatiliaji wa viwango vya ubora wa hewa wenye gharama nafuu ambao wataalam wanasema utaleta mabadiliko ya ufanyaji maamuzi kuhusu ongezeko la uchafuzi wa hewa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Ubora wa Hewa Duniani ya Mwaka 2021, Mji Mkuu wa Uganda, Kampala uliorodheshwa kati ya miji iliyochafuliwa zaidi, na viwango vya uchafuzi wa mazingira vilizidi kikomo cha Shirika la Afya Duniani(WHO) mara 5 hadi 7.

Kwa mujibu wa wanamazingira, vichocheo muhimu vya uchafuzi wa hewa mjini Kampala, ni barabara zisizo na lami, matumizi ya nishati yabisi ya majumbani, moshi kutoka kwenye magari, uzalishaji wa gesi asilia viwandani, na uchomaji wa wazi wa taka.

Kuishi kwenye uchafuzi wa hewa kuna matishio yanayohusiana na afya. Kwa mujibu wa WHO, takriban watu milioni 7 hufariki kutokana na uchafuzi wa hewa kila mwaka; Watu milioni 4.2 wanakufa kutokana na uchafuzi wa hewa wa nje ya nyumba na takriban milioni 3.8 kutokana na uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba. Kwa mujibu tafiti za kimataifa za mzigo wa magonjwa, uchafuzi wa hewa unachukua nafasi ya pili kwa kusababisha vifo. Nchini Uganda pekee, zaidi ya vifo 26,000 vinahusishwa na uchafuzi wa hewa peke yake kila mwaka

Mfumo huo wa ufuatiliaji viwango vya ubora wa hewa umeundwa na AirQo, kampuni ya programu inayowaleta pamoja wanasayansi 15 katika chuo kikuu hicho. Ina vipengele viwili, vifaa na programu. Vifaa vina sanduku la metali la ukubwa wa mitende, na vitambuzi vya hewa vilivyounganishwa. Sanduku limewekwa mahali panapohitajika, ambapo hutuma data kwenye wingu kupitia mtandao.

"Mfumo huo pia unaweza kushauri ipasavyo, kwa mfano, ikiwa hali ya hewa katika eneo fulani siyo nzuri, na kama una watoto ambao wana magonjwa ya kupumua kwa tabu, mfumo utashauri watoto wakae ndani hadi pale hewa ya hatari itakapokuwa safi," anasema Marvin Banda, mtengenezaji wa mifumo ya AirQo.

Banda anasema, mamlaka zinaweza pia kutumia taarifa za viwango vya ubora wa hewa kufanya maamuzi sahihi kuhusu udhibiti wa uchafuzi wa hewa.

Kwa mujibu wake, mfumo huo umejengwa ili kustahimili hali mbaya ya hewa barani Afrika na hivyo kifaa hicho kinaweza kupelekwa popote.

Hadi kufikia sasa AirQo imefunga vifaa 120 vya kufuatiliwa viwango vya ubora wa hewa kote nchini humo kwa msaada wa washirika na serikali ya Uganda.

Banda anasema, kupitia msaada huo kutoka kwa washirika, kuna mipango ya kupanua mfumo huo katika maeneo mengine ya Afrika, huku mji mkuu wa Kenya, Nairobi ukiwa wa kwanza.

Kifaa cha mfumo wa ufuatiliaji wa viwango vya ubora wa hewa kilichoundwa na AirQo kikionekana eneo la Chuo Kikuu cha Makerere huko Kampala, Uganda, Mei 31, 2022. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)

Watu wakifanya kazi ndani ya karakana ya AirQo katika Chuo Kikuu cha Makerere mjini Kampala, Uganda, Mei 31, 2022. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)

Msanidi wa programu akionyesha programu ya AirQo kwenye simu ndani ya karakana ya AirQo katika Chuo Kikuu cha Makerere mjini Kampala, Uganda, Mei 31, 2022. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)

Msanidi wa programu akifanya kazi ndani ya karakana ya AirQo katika Chuo Kikuu cha Makerere mjini Kampala, Uganda, Mei 31, 2022. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha