

Lugha Nyingine
Kenya yazindua programu ya simu ya lugha ya alama ili kuhimiza ujumuishwaji wa kijamii na kiuchumi
NAIROBI- Kenya Jumatano wiki hii imezindua programu ya simu ili kutoa huduma za ukalimani wa lugha ya alama kwa wakati halisi nchini Kenya ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukuza ujumuishwaji wa kijamii na kiuchumi.
Maureen Mbaka, Katibu Mkuu wa utawala katika Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT), Uvumbuzi na Masuala ya Vijana ya Kenya, amewaambia waandishi wa habari mjini Nairobi, kwamba programu (APP) ya assistALL ya simu itaziba pengo la mawasiliano kati ya watu wenye ulemavu wa kusikia na wahusika wengine katika sekta za afya, elimu ya juu, mfumo wa mahakama, huduma za serikali na fedha.
“AssistALL pia inatengeneza fursa za ajira kwa wakalimani wa lugha ya alama ambao wanaweza kujipatia vipato vya kudumu kwani programu hiyo inawaleta karibu na wateja wao bila kuzingatia utaratibu wa usafiri,” Mbaka amesema.
Takwimu zinaonyesha kuwa kwa sasa kuna zaidi ya watu 260,000 wenye ulemavu wa kusikia nchini Kenya.
Mbaka amebainisha kuwa programu hiyo ya simu italeta manufaa kwa watu wenye ulemavu kwa sababu mkalimani wa lugha ya alama anapatikana kwa kulipa shilingi 30 (kama senti 26 za Marekani) tu.
Amebainisha kuwa kwa makampuni na wataalamu, teknolojia hiyo ya simu itawawezesha kufikia watu wenye ulemavu wa kusikia ambao hapo awali hawakuzingatiwa wakati wa kupanga biashara.
Luke Muleka, Afisa Mtendaji Mkuu wa Signs Media ambayo imetengeneza programu hiyo, amesema kuwa teknolojia hiyo italeta mapinduzi katika namna ambavyo walemavu wa kusikia watashiriki katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Kenya kwa kuwawezesha kuishi kwa kujitegemea.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma