

Lugha Nyingine
Makala: Mchoraji wa katuni wa Tanzania na Mtangazaji wa redio atengeneza gari linalotumia nishati ya umeme
Ally Masoud akizungumza wakati wa mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua jijini Dar es Salaam, Tanzania, Aprili 7, 2022. (Picha na Herman Emmanuel/Xinhua)
DAR ES SALAAM - Mchana wa Aprili 2, 2022, Watanzania walipokelewa kwa habari njema zilizosikika kama muziki masikioni mwao -- ilikuwa siku ambayo raia mwenzao, mchora katuni, mtayarishaji na mtangazaji wa vipindi vya redio alizindua gari lake linalotumia nishati ya umeme lililotengenezwa nchini humo katika mji mkuu wa kibiashara wa Dar es Salaam.
Ilikuwa ni siku ambayo Ally Masoud mwenye umri wa miaka 49, na anayefahamika kwa jina maarufu la Masoud Kipanya, alitimiza ndoto yake iliyodumu kwa takriban muongo mmoja.
"Wakati ujao ni wa umeme," Masoud, baba wa watoto wanane, aliliambia Shirika la Habari la China, Xinhua mwanzoni mwa mahojiano ya hivi majuzi ambapo alielezea uvumbuzi wake mpya.
“Nimekuwa nikipokea simu nyingi kutoka kwa watu tangu nilipozindua gari langu la kutumia umeme, wakinishukuru kwa kuonyesha jinsi ambavyo kisichowezekana kinawezekana,” anasema Masoud huku akiachia tabasamu pana.
"Tangu Mwaka 2013 muda wote nimekuwa nikifikiria ni kwanini watu wengine wanatengeneza magari haya, meli, boti, vitu vizuri duniani. Inakuwaje sisi Waafrika hatuzalishi jinsi jamii nyingine zinavyozalisha? Sisi ni watumiaji zaidi, tunachukua zaidi, na sisi tunapokea tu. Tunaendesha magari lakini yanatengenezwa na watu wengine," anasema.
Anasema safari yake ya kutengeneza gari linalotumia umeme ilianza pale alipoanza kufikiria maswali hayo na kwanza akabuni lori dogo ambalo aliazimia kutengeneza.
“Kwa hiyo kuanzia Mwaka 2013 niliendelea kubadilisha na kuboresha na kurekebisha wazo hilo,” anasema Masoud.
Mwaka 2017, alianza kutafuta mahali ambapo angeweza kujenga au kukodi kwa mradi wake, hadi Mwaka 2019 ambapo Meneja wa Mkoa wa Dar es Salaam wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo, shirika ambalo ni la kiserikali alimpa sehemu moja katika eneo la Vingunguti, nje kidogo ya katikati ya mji.
"Mwezi Februari 2020 wakati nakaribia kuanza mradi wangu, UVIKO-19 uliingia. Kwa hivyo ilinibidi kuahirisha kuanza kwa mradi huo. Julai 18, 2020 nilianza mradi ambao ulituchukua miezi 21 kukamilika," anasema Masoud.
Anasema sehemu muhimu ya kutengeneza gari linalotumia umeme mbali na bodi ya gari ni injini. Kwa kuwa Tanzania haina teknolojia hii ya kutengeneza injini hiyo, kampuni ya Masoud iitwayo Kaypee Motors ilinunua kutoka nje ya nchi kwa bei nzuri. Chasisi na bodi la gari vilinunuliwa nchini Tanzania.
Anasema kampuni ya Kaypee Motors imekuwa ikipokea oda kadhaa, na kuongeza kuwa kampuni yake inajaribu kukusanya fedha kwa ajili ya mashine ili iweze kufanya uzalishaji kwa wingi.
"Tunapanga kununua mashine kutoka India au China kwa ajili ya uzalishaji kwa wingi. Na tutakapokuwa tayari tunapanga kutoa takriban magari 100 kwa mwezi," anasema.
Masoud anaamini kuwa siku zijazo ni za umeme. Anasema mtu anapozitazama nchi zilizoendelea ziko mbioni kuyaondoa magari yote yanayotumia nishati ya mafuta ifikapo Mwaka 2030 na 2035.
"Kwa hiyo lazima tujiunge na mbio hizo. Tunahitaji kuwa na mabingwa katika jitihada hii, tunahitaji kuwa na waanzilishi katika kuifanya," anasema.
Wakazi wakitazama gari linalotumia umeme la Ally Masoud lililotengenezwa nchini Tanzania katika uzinduzi uliofanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania, Aprili 2, 2022. (Picha na Herman Emmanuel/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma