

Lugha Nyingine
China kufanya safari mbalimbali kwenye anga ya juu Mwaka 2022
Roketi ya Long March-3B ikiwa imebeba satelaiti ya majaribio ya teknolojia ya mawasiliano ikiruka kutoka kwenye Kituo cha Kurusha Satelaiti cha Xichang katika Mkoa wa Sichuan, Kusini Magharibi mwa China Desemba 30, 2021. (Picha na Zheng Zhongli/Xinhua)
BEIJING - China itafanya safari sita za anga ya juu Mwaka 2022 ili kukamilisha ujenzi wa kituo chake cha anga ya juu na kushuhudia safari ya kwanza ya roketi ya Long March-6A, ikiwa ni roketi ya kwanza ya usafiri nchini humo inayoendeshwa kwa nishati yabisi na kimiminika.
Ma Tao, Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Anga ya Kampuni ya Sayansi na Teknolojia ya Anga ya Juu ya China (CASC), Jumatano wiki hii kwenye mkutano na waandishi wa habari ametangaza mpango wa China wa kurusha roketi.
CASC, kampuni inayotengeneza roketi nchini China na nguzo ya sekta ya anga ya juu nchini humo, imetoa Waraka wa Mwaka 2021 kuhusu Sayansi na Teknolojia ya Anga ya Juu ya China.
Kwa mujibu wa waraka huo, China ilifanya safari 55 za kurusha vyombo kwenye anga ya juu Mwaka 2021, na idadi hii inashika nafasi ya kwanza duniani, na jumla ya uzito wa vyombo vya anga ya juu vilivyorushwa ilifikia tani 191.19, ikiwa ni ongezeko la asilimia 85.5 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
CASC ilirusha vyombo vya anga ya juu 103 na roketi 48 angani Mwaka 2021, amesema He Yang, Mkurugenzi wa Taasisi ya Teknolojia ya Habari na Sayansi ya Anga ya Beijing, katika mkutano na waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa He, misheni nyingine za anga za juu zilizofaulu mwaka jana ni pamoja na kurushwa kwa roketi tatu za Kuaizhou-1A za kubeba satelaiti na kurushwa kwa roketi moja ya CERES-1.
Mwaka 2021, Dunia ilishuhudia misheni 146 za kurusha satelaiti kwenye anga ya juu, idadi ambayo ni kubwa zaidi tangu Mwaka 1957, huku vyombo 1,846 vikirushwa angani.
Kwa mujibu wa waraka huo, Marekani ilifanya safari 51 za kurusha vyombo kwenye anga ya juu Mwaka 2021, huku jumla ya uzito wa vyombo vya anga ya juu vilivyorushwa nchini humo ikifikia tani 403.34.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma