Mfumuko wa bei Marekani kwa Novemba wafikia kiwango cha juu katika miaka 39 iliyopita

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 24, 2021

Mteja akinunua bidhaa kwenye duka la mboga-mboga huko New York, Marekani, Desemba 7, 2021. (Xinhua/Wang Ying)

WASHINGTON – Kiwango cha mfumuko wa bei kinachofuatiliwa kwa karibu na Benki Kuu ya Marekani kilipanda kwa kasi zaidi katika Mwezi Novemba mwaka huu, ongezeko ambalo haijawahi kutokea katika kipindi cha miaka 39 iliyopita, na kuongeza shinikizo kwa Benki Kuu ya Marekani kukaza sera za fedha.

Benki Kuu ya Marekani imeeleza Alhamisi wiki hii kwamba, kielezi cha bei ya matumizi ya kibinafsi (PCE), ambacho ni kielezi kimoja cha mfumuko wa bei kinachopendekezwa na benki hiyo, kilipanda kwa asilimia 5.7 mnamo Novemba mwaka huu ikilinganishwa na mwaka uliopita, ikiwa ni kasi ya haraka zaidi tangu Julai 1982.

Kile kinachojulikana kama kielezi cha bei ya msingi ya PCE ambayo huondoa bei ya chakula na nishati, kiliongezeka kwa asilimia 4.7 kuliko mwaka uliopita, ikiwa ni kiwango cha juu cha lengo la ongezeko la mfumuko wa bei wa asilimia 2 uliokadiriwa na Benki Kuu.

Ripoti nyingine kutoka kwa Wizara ya Kazi ya Marekani pia inaonesha kuwa kielezi cha bei ya wanunuzi (CPI) kilipanda kwa asilimia 6.8 mnamo Novemba mwaka huu kutoka mwaka uliotangulia, ikiwa ni kasi ya haraka ambayo haijawahi kurekodiwa kwa karibu miaka 40 iliyopita.

Watu wakinunua bidhaa katika duka moja mjini New York, Marekani, Desemba 7, 2021. (Xinhua/Wang Ying)

"Kama vile CPI, mafanikio yalikuwa mapana zaidi, ambayo yametoa ishara ya hatari katika Benki Kuu," Diane Swonk na Yelena Maleyev, wataalam wa uchumi katika kampuni ya uhasibu ya Grant Thornton, wamesema Alhamisi wiki hii katika uchambuzi wao.

"Makubaliano miongoni mwa watumishi wa Benki Kuu ya Marekani ni kwamba hali tofauti zinasumbua zaidi minyororo ya ugavi, ikiwa ni pamoja na nguvukazi, kuliko mahitaji, na kwa hivyo kusababisha mfumuko mkubwa zaidi wa bei. Maafisa wa Benki wameacha nafasi ya kutosha ya kutathmini tena kama itahitajika, kabla ya kuanza kuongeza viwango vya riba, ambavyo tunatarajia kuanza Juni," wamesema wataalam hao.

Benki Kuu ya Marekani ilitangaza wiki iliyopita kwamba itaharakisha mwisho wa mpango wake wa ununuzi wa mali huku ikitarajia kuongeza riba kwa mara tatu mwaka ujao.

"Tunasitisha ununuzi wetu kwa haraka zaidi kwa sababu kutokana na shinikizo la juu la mfumuko wa bei na soko la ajira linaloimarika kwa kasi, uchumi hauhitaji tena uungaji mkono wa kisera," Mwenyekiti wa Benki Kuu Jerome Powell alisema wiki iliyopita.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha